• HABARI MPYA

    Sunday, August 12, 2012

    SIMBA KUMKOSA MBUYU TWITE, RAGE ANASTAHILI LAWAMA


    MWENYEKITI wa Simba SC, jana amekaririwa na vyombo vya habari nchini akimshutumu mtoto wa kigogo kimoja nchini kumshinikiza Rais wa APR ya Rwanda, Meja Alex Kagame ampeleke Yanga, beki Mbuyu Twite, wakati alikuwa amekwishasaini Simba na kupewa fedha.
    Na Mahmoud Zubeiry
    Rage amelalamika sana na akapiga hatua kubwa zaidi, akaanza kuwakashifu viongozi wa Yanga, wana fedha chafu za EPA.
    Yote haya yanakuja baada ya kuzidiwa kete katika kuwania saini ya Twite. Namfahamu Rage na hii ndio desturi yake. Anapopandisha jazba huweza kusema lolote, bila ya kujali chochote.
    Kabla ya kuzungumzia sakata la mchezaji huyo, nianze kwa kumuelewesha tu Rage, asitazame boriti kwenye jicho la wapinzani wake, Yanga akasahau kibanzi kilichopo kwenye jicho lake.
    Rage anafahamu fika, mambo ambayo yako mahakamani huwa hayajadiliwi nje ya Mahakama na hakuna asiyefahamu kwamba suala la wizi wa fedha kwenye Akaundi ya Madeni ya Nje (EPA), lilifikishwa mahakamani na baadhi ya waliokutwa na hatia, hivi sasa wanatumikia kifungo jela.
    Na hivi karibuni, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alipokutana na Wahariri wa vyombo vya Habari nchini, Ikulu mjini Dar es Salaam, amerudia kusema juu ya hilo, kwamba serikali haimlindi yeyote na ilizikabidhi mamlaka husika zichukulie hatua hilo na kwa kuwa mamlaka hizo ni huru, hawawezi kuziingilia.
    Sasa inakuwa jambo la ajabu, Rage anapothubutu kumuhukumu mtu mwingine nje ya Mahakama juu ya EPA.
    Ni sawa tu na leo hii, atokee mtu aanze kumzungumzia yeye kuhusu dola 40,000 za Yanga za mwaka 1998 alizochukua CAF (Shirikisho la Soka Afrika) au tuhuma nyingine lukuki za ubadhirifu wa mali za Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa Shirikisho, TFF), atakuwa hamtendei haki, kwa sababu Mahakama ilikwishaamua.
    Awali, Rage alihukumiwa kifungo jela, kabla ya kutoka kwa msamaha wa Rais, baadaye akaenda Mahakama ya Rufaa, kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, akafanikiwa, mahakama ikamsafisha na ndio maana leo ni Mbunge na Mwenyekiti was Simba, vinginevyo asingeweza kupata haki ya kugombea hata Ukatibu Kata.
    Naomba niwaombe radhi wasomaji wangu na Rage pia, kwa kukumbushia suala la dola 40,000 na kifungo cha Rage kabla ya kutoka kwa msamaha wa Rais, kwa kuwa natambua si busara kuzungumzia mambo ambayo yamefikishwa Mahakamani.

    MTOTO WA KIGOGO;
    Hajamtaja jina, lakini dhahiri hapa anazungumziwa Ridhiwani, mtoto wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Nani asiyejua kama Ridhiwani ni Yanga na Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga na sidhani kuna dhambi katika hilo, ikiwa Waziri Mkuu wa zamani, ‘Simba wa Vita’, Mzee Rashid Mfaume Kawawa alikuwa Simba.
    Simba na Yanga ni timu za Watanzania, na ndio maana Profesa Juma Athumani Kapuya, Rage mwenyewe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Zitto Kabwe, Iddi Azzan na wengine miongoni mwa vigogo wa nchi yetu ni Simba.
    Kama Ridhiwani alijaribu kuisaidia Yanga, timu yake kuna dhambi gani, ikiwa mwaka 2005 Kapuya aliisaidia timu yake, Simba SC kutompoteza beki Victor Costa, ingawa alikuwa amesaini Yanga na kupewa fedha?
    Mimi namheshimu rais wetu, Kikwete na sidhani kama ana muda wa kushughulika na ‘upuuzi’ wa Simba na Yanga- lakini kama mzazi pia ambaye anatambua Ridhiwani kijana wake naye ni baba wa familia pia, ana uhuru wake katika mambo yake. Hawezi kumuingilia. 
    Yanga imepitia wakati mgumu na Kikwete yupo pale pale Ikulu na hajaonyesha hata dalili za kutaka kuwasaidia Yanga. Kikwete akiwa Ikulu, alileta kocha kwa ajili ya timu ya taifa, turudi enzi zile Rage na Samuel Sitta wakiwa CDA, walilitumia shirika hilo kwa manufaa ya timu ya taifa au Simba? Watu wanakumbuka haya mambo ndio maana namtahadharisha Rage, asiangalie boriti kwenye jicho la wapinzani, wakati jicho lake lina kibanzi.     
    Mambo ya kuchafuana si mazuri na yamepitwa na wakati- Rage kama ameamua kuwa Mwenyekiti was Simba, basi apambane na changamoto zote bila ya kumnyooshea mtu kidole na kwa kweli umefika wakati Rage aachane na ‘Saisa za Majitaka’, kwanza hata umri wake tu haumruhusu tena kufanya mambo kama hayo, amekwishakuwa mtu mzima sasa.
    Huyo Ridhiwani kama ndio staili yake hiyo kutisha watu, kwa nini asianzie hapa nyumbani kuwatisha viongozi wa Azam katika suala la Mrisho Ngassa wampeleke Yanga? Rage amewahi kupewa onyo kali na TFF kwa kosa la kutoa kauli za uchochezi na ajabu hajaacha, kwani kauli zake dhidi ya mtoto wa kigogo ni za uchochezi. Ni za hatari.

    SAKATA LA MBUYU TWITE
    Kama kuna mtu wa kwanza wa kulaumu juu ya Simba kumpoteza Mbuyu Twite, basi ni Aden Rage. Kwa nini? Alipofika Kigali, baada ya kumpa fedha beki huyo na kumsainisha mkataba, alijua fika na Yanga nao wanamfuatilia mchezaji huyo.
    Yanga wale wale, waliomchukua Kevin Yondan na kumsainisha mkataba, wakati tayari amesaini mkataba (kwa mujibu wa Simba) wa kuendelea kuichezea klabu yake, Simba SC.
    Ajabu Rage akijua kabisa, Yanga si waungwana, akamuacha Twite Kigali, yeye akawahi Mkutano Mkuu na baadaye shughuli za Bunge, huku nyuma Yanga wakafanya ambacho kinamsababisha leo yeye azungumze huku mapovu yanamtoka mdomoni.
    Rage alitakiwa arudi Dar es Salaam na Mbuyu Twite, apokewe na maelfu ya wana Simba halafu tungeona kama angethubutu kusaini Yanga. Rage pamoja na uzoefu wake wote katika masuala ya usajili na fitina za mpira, hapa alichemka na badala ya kutafuta mchawi, ni vema akajilaumu mwenyewe.
    Nimependa alivyomalizia mazungumzo yake jana, alisema wao watatafuta mchezaji mwingine mzuri na anachoomba tu, Simba warudishiwe fedha zao, kiasi cha dola 40,000 hivi, pamoja na gharama za nauli, kwake, mchezaji mwenyewe na mawakili waliotayarisha mkataba aliosaini Twite. Safi.

    TUACHE UHUNI KATIKA SOKA YETU:
    Soka yetu imegubikwa na mambo ya kihuni, ambayo wenyewe wanayaita ya kimjini, ambayo siku zote mimi tangu nipo DIMBA, kuanzia Mwandishi hadi Mhariri, nilikuwa nayapinga vikali, kwa sababu najua athari zake ni kuididimiza soka yetu.
    Leo Simba wakilia kuhusu Twite, Yanga watawaambia; Mnakumbuka Costa? Na bado historia inaanzia mbali tangu ya 1960, Simba na Yanga zilikuwa zinapokonyana wachezaji.
    Ila katika dunia ya leo, inayotawaliwa na utaalamu, taratibu, kanuni na sheria, kwa nini tuendelee kuyalea mambo kama haya?
    Siyo tu sijapendezewa na staili waliyoitumia Yanga kumsajili Twite, lakini pia sijapenda staili waliyotumia Simba kumsajili Ramadhan Chombo ‘Redondo’, ambayo leo inawaliza Azam.
    Huo ni upande mmoja, upande wa pili, kuhonga wachezaji wa timu pinzani na marefa- hili pia silipendi na ni sehemu ya uhuni, ambao unapoteza maana halisi ya soka ambayo FIFA wanaitaka. Soka ya kiungwana. Hayo yalikuwa mapitio tu, leo ujumbe wangu ulikuwa Mh. Alhaj Rage; asikumuke EPA tu, kuna dola 40,000 za Yanga, je watu wakumbushie hizi? Nawatakia saumu njema na kwa ujumla mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhan inshaallah.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA KUMKOSA MBUYU TWITE, RAGE ANASTAHILI LAWAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top