• HABARI MPYA

    Friday, April 24, 2015

    YANGA HESHIMA KWAO, RUVU ATANDIKWA 5-0…MSUVA APIGA MABAO YA HATARI, TAMBWE, SHERMAN…

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    ZIMEBAKI dakika 90 Yanga SC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambao kwa sasa taji lake limehahifadhiwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Hiyo inafuatia Wana Jangwani hao kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 jioni ya leo dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC ya kocha Mholanzi, Hans va der Pluijm, sasa inatimiza pointi 52, baada ya kucheza mechi 23 na katika mechi tatu zilizobaki itahitaji pointi tatu kufikisha 55, ambazo haziwezi kufikiwa na mabingwa watetezi, Azam FC.
    Winga Simon Msuva alitimiza mabao 16 leo baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi huo, na kuzidi kuwaacha mbali washindani wake katika mbio za ufungaji bora, Warundi Amisi Tambwe mwenye mabao 11, Didier Kavumbangu na mzalendo Rashid Mandawa wenye mabao 10 kila mmoja.     
    Wafungaji wa mabao mawili kila mmoja katika mchezo wa leo, Simon Msuva kulia na Kpah Sherman kushoto wakipongezana leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

    Ni Msuva aliyefungua ‘biashara’ leo baada ya kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 14, kwa kichwa akimalizia kona iliyopigwa na Haruna Niyonzima.
    Mliberia Kpah Sean Sherman akafunga bao la pili dakika ya 24 akimalizia kona iliyochongwa na Msuva.
    Refa Isihaka Shirikisho wa Tanga alimuonyesha kadi ya njano beki ‘Mndava’ George Michael dakika ya 26 baada ya kumpiga kiwiko Mrisho Ngassa wa Yanga SC.
    Msuva akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika 44 kwa kichwa tena akimalizia krosi ya Niyonzima.
    Katika kipindi hicho cha kwanza, shambulizi la maana zaidi walilofanya Ruvu ni dakika ya 42, baada ya beki Kevin Yondan kuokoa mpira uliopigwa na Baraka Mtuwi uliokuwa unaelekea nyavuni.
    Kipindi cha pili, Yanga SC walirejea na kasi yao nzuri na kufanikiwa kupata bao la nne lilofungwa na mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Tambwe baada ya kumhadaa kipa Abdallah Rashid kufuatia pasi ya Kpah Sherman dakika ya 57.
    Awali ya hapo, almanusra Ngassa afunge dakika ya 50 kama si shuti lake kugonga mwamba na kuondoshwa kwenye hatari na Salvatory Ntebe.
    Mrisho Ngassa akimhadaa beki wa Ruvu, Abdul Mpambika katika mchezo wa leo
    Juma Abdul akimtoka beki wa Ruvu, Abdu Mpambika
    Amissi Tambwe kulia akimiliki mpira pembeni ya beki wa Ruvu, Salvatory Ntebe

    Mwita John alikaribia kuifungia Ruvu dakika ya 65, baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga SC, lakini shuti lake likatoka nje sentimita chache kutoka nguzo ya lango.
    Sherman aliifungia Yanga SC bao la tano dakika ya 67 kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Juma Abdul. 
    Mwita John akapoteza nafasi nyingine nzuri ya kufunga dakika ya 70 akiwa amebaki yeye na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.
    Yanga SC ilipata pigo dakika ya 87 baada ya kiungo wake mkabaji, Said Juma 'Makapu' kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa Mbrazil, Andrey Coutinho.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa, Juma Abdul, Oscar Joshua/Edward Charles dk68, Rajab Zahir, Kevin Yondani, Said Juma/Andrey Coutinho dk87, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman/Hussein Javu dk77.
    Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Michael Aidan, Abdul Mpakala, George Osei, Hamisi Suleiman, Salvatory Ntebe, Raphael Kyala/Juma Nade dk78, Ally Khan, Yahya Tumbo, Baraka Mtuwi/Juma Mpakala dk49 na Abdulrahman Mussa/Mwita John dk49.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA HESHIMA KWAO, RUVU ATANDIKWA 5-0…MSUVA APIGA MABAO YA HATARI, TAMBWE, SHERMAN… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top