• HABARI MPYA

    Monday, April 20, 2015

    FUNGUA MACHO CHRISTIAN BELLA KABLA MCHEZO HAUJAGEUKA

    JUMAMOSI ya juzi, Christian Bella alifanya onyesho kubwa ndani ya Escape One jijini Dar es Salaam, onyesho lililotajwa kama tukio la mapinduzi mapya ya muziki wa dansi lakini yakiwa yamesindikizwa na wasanii wengi wa bongo fleva.
    Wako watu flani wakauliza “Ni mapinduzi mapya ya dansi au ya bongo fleva?” Ni swali ambalo sitaki kulijengea hoja wala kulitolea majibu, ni mada pana inayohitaji uwanja mpana na wachambuzi wapana.
    Lakini yote kwa yote, ni onyesho lililobeba msisimko wa aina yake, jiji la Dar es Salaam likatingishika kwa promo za usiku huo wa kipekee na mwisho wa siku watu wakapata burudani ya kipeee.
    Christian Bella ni mwimbaji mwenye uwezo wa kipekee, jina lake likachomoza bila kutumia nguvu pindi tu alipokanyaga ardhi ya Tanzania miaka kadhaa iliyopita.

    Wakati Akudo Sound inasukwa upya na kuitwa Akudo Impact katikati ya miaka ya 2000, wakaletwa wasanii kutoka DRC (Zaire) akiwemo Bella, lakini huwezi kuamini aliyekuwa anatajwa sana ni Alain Kabasele (tukiambiwa ni mtoto wa Pepe Kalle).
    Bella hakuwa gumzo, mpango mzima ulikuwa ni mtoto wa Pepe Kalle, kila mtu akasubiri kumsikia mtoto wa Pepe Kalle, hakuna kingine zaidi ya hicho lakini pindi sauti ya Christian Bella iliposikika kwenye wimbo wao wa kwanza “Walimwengu” tena kwenye ‘pande’ ambalo lilikuwa halina ujumbe wowote unaoendana na maudhui ya wimbo, watu wakabaini kuwa hiyo ndio sauti ya dhahabu.
    Alipotoa wimbo wake “Yako Wapi Mapenzi” ghafla wimbo huo ukawa kama wimbo wa taifa na kuanzia hapo Bella akawa matawi ya juu, kila kazi yake iliyofuata baada ya hapo ikaibuka kuwa bidhaa nzuri masikioni mwa mashabiki wa muziki.
    Bella kwa sasa yuko na Malaika Music Band, bendi iliyozinduliwa rasmi Novemba mwaka 2013 pale Mzalendo Pub Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
    Christian Bella akatua Malaika na nyimbo mbili “Nakuhitaji” na “Mtu wa Watu” zikafanya vizuri hasa “Nakuhitaji” na haikushangaza pale alipotwaa tuzo ya mtunzi bora wa nyimbo za dansi kupitia Kili Music Awards 2013/2014.
    Lakini nasikitika sana kuwa hadi leo hii Malaika Band bado inaishi kwa nyimbo hizo mbili tu, huku “Nakuhitaji” peke yake ndio ukiwa katika video – Mwaka mmoja na nusu nyimbo mbili tu?
    Naskia pale studio za C9 Kinondoni kuna nyimbo za Malaika za kutosha albam nzima lakini kwa zaidi ya miezi sita zinasubiri sauti ya Bella tu, kila kitu kiko tayari isipokuwa sauti ya Bella.
    Mwaka jana Bella ametoa kazi yake binafsi “Nani Kama Mama” ikafanya vizuri sana, mwaka huu katoa tena kazi yake binafsi “Nashindwa” lakini Malaika bado wanasotea nyimbo mbili pamoja na kutegemea nyimbo binafsi za Bella kwenye maonyesho yao.
    Kwanini Bella hana haraka ya kutengeneza nyimbo mpya za Malaika Band? wako waimbaji wawili watatu pale wenye uwezo wa hali ya juu ambao ndani ya mwaka mmoja na nusu waliodumu na bendi hiyo tayari walipaswa kuwa na majina makubwa na hata uwezo wa kuendesha Malaika bila Bella pale anapokuwa nje ya nchi.
    Bella ni mwimbaji na msanii mkubwa sana, anapaswa sasa kuitengeneza Malaika Band itakayojitegemea kwa nyimbo zake bila kutegemea msururu mrefu wa nyimbo binafsi za Bella alizozitengeneza nje ya bendi – atengeneze Malaika itakayokuwa na nyimbo zinazojulikana. Hakuna ubishi kuwa kwasasa Malaika ndio bendi kijogoo kwa maana ya kujaza mashabiki ukumbini hivyo basi kitendo cha bendi hiyo kuwa na nyimbo mbili tu redioni kwa zaidi ya miezi 17 hakikubaliki.
    Malaika inakosa vigezo vya kushiriki Kili Music Awards 2014/15 kuanzia wimbo bora wa dansi, bendi bora ya dansi, mwimbaji bora wa dansi na hata mtunzi bora wa dansi (ingawa Bella binafsi anaweza kuingia kwa mlango wa bongo fleva kupitia wimbo wake Nani Kama Mama) – hii ni kwasababu tu bendi hiyo imeshindwa kuingiza hata wimbo mmoja redioni tangu tuzo za mwaka 2013/14 zilipomalizika. Fungua macho Bella kabla mchezo haujageuka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FUNGUA MACHO CHRISTIAN BELLA KABLA MCHEZO HAUJAGEUKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top