• HABARI MPYA

    Sunday, March 29, 2015

    SAMATTA AINUSURU STARS KUPIGWA NA MALAWI KIRUMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
    BAO la Mbwana Ally Samatta dakika ya 76, jioni ya leo limeinusuru Tanzania kulala mbele ya Malawi baada ya kutoa sare ya 1-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Mshambuliaji huyo wa TP Mazembe ya DRC, Samatta alifunga bao hilo akiwa katikati ya mabeki wawili wa The Flames, baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Haroun Chanongo.   
    Esau Kanyenda alianza kuifungia Malawi dakika ya tatu tu ya mchezo, baada ya kuuwahi mpira uliorudi kufuatia kona ya Haray Nyirenda kuzua kizaa langoni mwa Taifa Stars.
    Mbwana Samatta akishangilia baada ya kuifungia Stars bao la kusawazisha dakika za lala salama

    Stars ilishindwa kuupasua ukuta wa The Flames kipindi cha kwanza na nafasi pekee nzuri ilikuwa dakika ya 14, lakini shuti la Samatta likaokolewa na kipa McDonald Marava.
    Zaidi ya hapo, Amri Kiemba alipiga nje dakika ya 17 akiwa kwenye nafasi nzuri na Shomary Kapombe akapiga juu ya lango dakika ya 19 baada ya krosi nzuri ya Haroun Chanongo.
    Kipindi cha pili, Stars ilibadilika baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Mart Nooij akiwatoa viungo Amri Kiemba na Chanongo na kuwaingiza Ngassa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Haroun Chanongo akimtoka beki wa Malawi Chimango Kaira
    Thomas Ulimwengu akigombea mpira na beki wa Malawi, Lambikan Mzava

    Shomary Kapombe akimiliki mpira katikati ya mabeki wa Malawi, Lambikan Mzava kulia na Joseph Kamwendo kushoto

    Stars ilipiga ziara kwenye lango la Malawi kwa dakika zote tano za mwisho kusaka bao la ushindi, lakini bahati haikuwa yao.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Mwadini Ali, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Aggrey Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Mwinyi Kazimoto, Haroun Chanongo/Mrisho Ngassa dk59, Amri Kiemba/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk68, Thomas Ulimwengu/John Bocco dk81 na Mbwana Samatta.
    Malawi; MacDonald Marava, Joseph Kamwendo, Haray Nyirenda, Limbakan Mzava, Chimango Kaira, Francis Mulimbika, John Langes, John Banda/Frank Banda dk63, Mucium Mhone, Peter Wadabwa na Essau kanyenda/Chikoti Chirwa dk79.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AINUSURU STARS KUPIGWA NA MALAWI KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top