• HABARI MPYA

    Sunday, March 01, 2015

    KWA MTAJI HUU, TUTARAJIE SOKA YA AFRIKA ITAKUWA KWA NAMNA ZIPI?

    WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC jana wameaga mashindano hayo, baada kufungwa mabao 3-0 na wenyeji El Marreikh ya Sudan katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali uliofanyika Uwanja wa Marreikh mjini Khartoum.
    Marefa wa mchezo huo kutoka Zambia Wellington Kaoma aliyesaidiwa na Romeo Kasengele na Amos Nanga walionekana wazi kuiuma Azam FC katika mchezo huo.
    Pamoja na kupewa penalti ambayo ilipigwa na Mghana Augustine Okrah na kuokolewa na kipa Aishi Manula, Merreikh ilimaliza dakika 45 za kwanza inaongoza 1-0 lililofungwa Bakri dakika ya 16.

    Kipindi cha pili marefa wa Zambia waliongeza mbeleko kwa Merreikh na ikafanikiwa kupata mabao mawili zaidi yaliyofungwa na Ahmed Abdallah dakika ya 85 na Alan Wanga dakika ya 90.
    Azam FC imetolewa kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kwa kujua mbinu walizopanga na marefa hao, Merreikh walizuia mchezo huo usionyeshwe na Televisheni yoyote.
    Mchezo wa kwanza Dar es Salaam, Uwanja wa Azam Comoplex, Chamazi, ulionyeshwa na Televisheni na dunia iliushuhudia.
    Lakini kuelekea mchezo wa marudiano, Azam FC kama klabu ilikwenda na kamera kwa ajili ya kuurekodi mchezo huo na mazoezi yake kwa ujumla nchini Sudan, ila kwa bahati mbaya vifaa hivyo havikuruhusiwa kuingia nchini humo.
    Vilizuiliwa Uwanja wa Ndege wa Khartoum na Merreikh mapema ilitangaza hakuna kamera ya Televisheni itakayoruhusiwa kuingia uwanjani- na kweli haikuingia kamera na mchezo haukuonyeshwa.
    Kinachofuatia ni kile kilichoshuhudiwa na Waandishi wa Habari wa Tanzania waliokuwa huko, kwamba Azam FC ilionewa na marefa, wachezaji wake walipigwa na mayai wakati wanaingia uwanjani, timu ilipewa basi bovu na kufanyiwa hila nyingine zisizo za kiuanamichezo.
    Wazi hapa inaonekana kuna mchezo mchafu ambao marefa wa Zambia waliupanga na Merreikh kuhakikisha kwa vyovyote Azam inatolewa.
    Dhamira imetimia. Azam FC imetolewa, Merreikh inasonga mbele, lakini vipi kuhusu mustakabali wa soka ya Afrika?
    Azam FC ni timu mpya iliyoanzishwa na bilionea mkubwa barani Afrika, Mtanzania Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa kwa ushawishi wa wanawe, ambaye lengo lake ni kuonyesha mkono wake katika kuchangia maendeleo ya soka barani.
    Amejenga akademi kubwa pale Chamazi, anazalisha vipaji ambavyo tayari ni tegemeo la soka ya Tanzania na kwenye makabati yake kuna makabrasha ya mikakati zaidi.
    Anavumilia urasimu na unafiki wa soka ya Tanzania unaotaka kila siku Simba na Yanga ziwe juu, kwa matumaini siku moja mambo yatabadilika, lakini kwenye michuano ya Afrika nako anakutana na upuuzi mwingine.
    Bakhresa anafanya jitihada zenye kuonekana kabisa kuisaidia soka ya Tanzania na Afrika kwa ujumla, lakini mwisho wa siku anakutana na maumivu.
    Anakutana na mambo ambayo hayawezi kutokea kabisa Ulaya. Barcelona hawawezi kuzuia kamera za Manchester City kuingia Uwanja wa Camp Nou kwa ajili ya mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya.
    Hilo linawezekana Afrika, Merreikh inaweza kuzuia mchezo wake usionyeshwe ili iweze kutekeleza azma zake.
    Bakhresa na familia yake wana shida gani na mpira wa Afrika- na tutarajie nini ikiwa wataamini kuna udhalimu mkubwa katika mchezo huo barani?
    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipata taarifa hizo mapema- lakini viongozi wake hawakuonekana kushtushwa kwa sababu wanazojua wenyewe.
    Lakini dunia inajua, Mwenyekiti wa Kamati ya Marefa ya CAF, Magdi Shams El Din anatoka Sudan, dunia inajua Sekretarieti ya CAF inaundwa na Waarabu wa Misri, ambao ni maswahiba na Wasudan.
    Kwa muda mrefu, timu za Misri na Kaskazini mwa Afrika zimeonekana kufanyiwa upendeleo wa wazi na CAF ikiwemo kupangiwa ratiba nzuri mwanzoni dhidi ya timu dhaifu ili zifanye vizuri na haishangazi mabingwa mara nyingi wa michuano yake wanatoka Cairo, Al Ahly na Zamalek.
    Lakini ukienda kwenye Kombe la Dunia huoni makali yao- Cameroon, Senegal na Ghana ndiyo pekee wamewahi kufika Robo Fainali ya michuano hiyo ya FIFA, kwa nini si hao wababe wa michuano ya CAF?
    Tunapoelekea ni kubaya kwa mtindo huu na hakuna ajabu soka ya Afrika, badala ya kukua itazidi kudidimia. Poleni Azam FC, pole Bakhresa na familia yake, lakini hii ni aibu kubwa kwa soka ya Afrika. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA MTAJI HUU, TUTARAJIE SOKA YA AFRIKA ITAKUWA KWA NAMNA ZIPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top