• HABARI MPYA

    Monday, March 02, 2015

    AZAM FC YAREJEA NA ‘MANUNDU’ YA SUDAN, YAELEKEZA NGUVU LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Azam FC kimerejea jana jioni kutoka Khartoum, Sudan baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kufuatia kufungwa mabao 3-0 na El Merreikh ya Sudan katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali uliofanyika Uwanja wa Marreikh mjini Khartoum juzi.
    Mara baada ya kuwasili Dar es Salaam, wachezaji walipewa ruhusa ya kwenda kwenye familia zao kabla ya kukutana leo kwa ajili ya mazoezi, kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

    Mabingwa wa Tanzania Bara, sasa wanaelekeza nguvu zao katika kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu na Jumamosi watamenyana na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, wakihitaji ushindi kupunguza idadi ya pointi wanazozidiwa na vinara Yanga SC.
    Baada ya mechi 16 kila timu, Yanga SC ipo kileleni kwa pointi zake 31, wakati Azam FC ina pointi 27.   
    Katika mchezo na Merreikh, Azam wamelalamika kuonewa na marefa wa Zambia, Wellington Kaoma aliyesaidiwa na Romeo Kasengele na Amos Nanga.
    Pamoja na kupewa penalti iliyopigwa na Mghana Augustine Okrah na kuokolewa na kipa Aishi Manula, Merreikh ilimaliza dakika 45 za kwanza inaongoza 1-0 lililofungwa Bakri dakika ya 16.
    Kipindi cha pili marefa wa Zambia waliongeza mbeleko kwa Merreikh na ikafanikiwa kupata mabao mawili zaidi yaliyofungwa na Ahmed Abdallah dakika ya 85 na Alan Wanga dakika ya 90.
    Azam FC inatolewa kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAREJEA NA ‘MANUNDU’ YA SUDAN, YAELEKEZA NGUVU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top