• HABARI MPYA

    Wednesday, January 21, 2015

    YANGA NA AZAM KUJILIPIA HOTELI UGENINI MICHUANO YA AFRIKA, AGIZO LA CAF HILO

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limefanyia marekebisho kanuni zake za michuano ya ngazi ya klabu kwa upande wa malazi ambapo sasa timu zitachagua na kujilipia zenyewe hoteli zinapokuwa kwenye mechi za ugenini.
    Kabla ya marekebisho ya kanuni hiyo, timu ngeni ilikuwa ikilipiwa hoteli na timu mwenyeji kwa msafara usiozidi watu 25. CAF ilikuwa imepitisha hoteli maalumu katika kila nchi ambapo mwenyeji alitakiwa kuziweka timu ngeni.
    Kwa marekebisho hayo, Chama cha Mpira wa Miguu cha nchi mwenyeji kitakuwa na wajibu wa kuitafutia hoteli timu ngeni iwapo tu kitaombwa kufanya hivyo, lakini jukumu la kulipia malazi litakuwa la timu yenyewe.
    Kikosi cha Yanga SC kitakachoheza Kombe la Shirikisho

    Mwaka huu Tanzania inawakilishwa na timu mbili za Azam na Yanga katika michuano ya CAF. Azam inacheza Ligi ya Mabingwa (CL) ambapo itaanzia nyumbani Februari 15 mwaka huu kwa kuikaribisha El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
    Nayo Yanga itacheza michuano ya Kombe la Shirikisho (CC), na imepangiwa kucheza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya BDF IX ya Botswana. Mechi hiyo itafanyika Februari 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NA AZAM KUJILIPIA HOTELI UGENINI MICHUANO YA AFRIKA, AGIZO LA CAF HILO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top