• HABARI MPYA

    Wednesday, October 01, 2014

    BODI YA LIGI IMEKUJA KUIBORESHA, AU ‘KUIKONGOLOA’ LIGI KUU?

    CHOMBO huru cha kuendesha Ligi Kuu Tanzania Bara ni jambo ambalo lilikuwa kilio cha wadau wengi, hususan klabu zenyewe.
    Pamoja na ukweli huo, wazo hilo lilipata upinzani mkali kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)- chini ya Rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga kabla ya kumpisha Jamal Malinzi aliye madarakani hivi sasa.
    Tenga alikuwa anakataa uletwaji haraka wa chombo hicho, akisistiza wakati mwafaka ukifika kitakuja.
    Lakini kutokana na presha ya wadau na vyombo vya Habari, hatimaye Tenga alikubali uundwaji wa chombo huru cha kuendesha ligi nchini.

    Tenga, alianza na Kamati ya Ligi na baadaye ikaundwa bodi rasmi ya ligi hiyo, ambayo inasimamiwa na klabu zenyewe.
    Wazo lilipokewa kwa furaha na klabu wakiamini sasa taswira ya Ligi Kuu itakuwa nzuri zaidi kwa ujumla na thamani yake itaongezwa.
    Klabu zilipiga kura kuchagua viongozi wa Bodi kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka jana, chini ya Mwenyekiti Hamad Yahya wa Kagera Sugar na Sheikh Said Muhammad wa Azam FC akawa Makamu wake.
    Mmoja wa wana harakati wa uundwaji wa chombo huru cha ligi nchini, Silas Mwakibinga akaajiriwa kuwa Mtendaji Mkuu wa bodi.
    Unaweza kusema maisha ya bodi yanaanza rasmi Oktoba mwaka jana na mwishoni mwa mwezi huu itatimiza mwaka mmoja, lakini je imeonyesha dalili ya kuibadilisha ligi yetu na kuwa bora zaidi kama ilivyotarajiwa?
    Bila kupinda kona au kung’ata ulimi- Bodi ya Ligi hadi sasa bado haijaonyesha mwelekeo wowote wa kuibadilisha ligi yetu zaidi ya kuonekana kama mzigo.
    Kuendesha Bodi hiyo ni gharama na fedha za uendeshwaji wake zinatoka kwenye fungu la udhamini wa Ligi Kuu, kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo, Vodacom na kampuni ya Azam Media Limited, ambayo imeuziwa haki za matangazo ya Televisheni.
    Ofisi zao zipo kwenye majengo mapya ya gharama kubwa katikati ya mji, lakini ufanisi wao ni mdogo mno.
    Mwakibinga anapiga sana kelele kwenye vyombo vya habari kuhusu viwanja na mikwara ya kuvifungia, lakini Ligi Kuu imeendelea kuchezwa kwenye viwanja vibovu. 
    Klabu bado zinatumia vifaa kwa maana ya jezi na kadhalika vyenye ubora wa chini. Baadhi ya viwanja kumekuwa na malalamiko ya ligi kuchezwa katika mazingira hatarishi wakati mwingine kukiwa hakuna hata gari la kubebea wagonjwa.
    Kabla ya ujio wa bodi, tayari tulikwishaingia kwenye utaratibu wa kuwa na wachezaji bora wa mwezi, lakini tangu wameingia madarakani ukatoweka hadi jana walipokurupuka kumtaja Anthony Matogolo wa Mbeya City.
    Ligi Kuu imeanza Septemba 20 na kila timu imecheza mechi mbili tu hadi sasa, je huyo ni mchezaji wa mwezi au wiki mbili? Bodi ilitakiwa kumtaja mchezaji bora wa mwezi baada ya Oktoba 20.
    Lakini pamoja na hayo, Matogolo amefanya kipi ashinde tuzo hiyo, wakati Mbeya City imetoa sare mechi moja na kushinda moja kwa mbinde 1-0, bao la penalti ya utata zote nyumbani wakati kuna mchezaji amefunga mabao mawili kila mechi Azam FC, Didier Kavumbangu?
    Au ndiyo tuseme Mwakibinga analipa fadhila nyumbani kwao Mbeya? 
    Wadau walitarajia Bodi ya Ligi Kuu ingesaidia kupatikana wadhamini zaidi, lakini matokeo yake wanamaliza mwaka hakuna jipya.
    Kana kwamba hiyo haitoshi- yanaanza kuibuka mambo ya ‘kiswahili’ ndani ya bodi hiyo, ya kuvujisha mawasiliano baina yao na Kamati ya Utendaji ya TFF.
    Huo ni ukosefu mkubwa wa uadilifu- sitaki kuamini kwamba TFF inaweza ikawaandikia bodi barua ya maombi ya fedha, halafu wenyewe wakavujisha kwenye vyombo vya habari.
    Wazi mawasiliano hayo yatakuwa yamevuja kutokea huko kwenye bodi- lakini huo ni ukosefu wa uadilifu- kwani walipaswa kuwa na mjadala tu na TFF wakamalizana kimya kimya.
    Hakuna asiyejua TFF ina mzigo mkubwa wa kuendesha timu za taifa kuanzia za vijana na wanawake- ukiachilia mbali ya wakubwa, Taifa Stars yenye udhamini wa TBL.
    Bodi ya Ligi pamoja na kuwa chombo huru cha kuendesha mashindano hayo, lakini kipo chini ya TFF. 
    Tutacheza Ligi na kila kitu, lakini mwisho wa siku ustawi wa timu ya taifa ndiyo fahari ya Mtanzania- na ili tuwe na timu bora ya taifa, lazima tuanzie chini katika kutengeneza timu bora za vijana.
    Yenyewe bodi ya ligi imeshindwa kutuletea ligi imara ya vijana, japokuwa klabu zinashinikizwa kuingia gharama ya kuunda timu za vijana.
    Bodi ya Ligi Kuu kuanza kuweweseka kwa kuombwa asilimia tano maana yake imekwishajiridhisha litakuwa pigo kubwa kwao kwa sababu haina uwezo wa kuingiza fedha mpya kwenye bodi hiyo.
    Hali jinsi ilivyo kwa sasa ndani ya Bodi ya Ligi, ni kinyume kabisa na matarajio ya wadau- katika wiki ya pili tu tangu kuanza kwa ligi hiyo, Ratiba inafumuliwa kwa sababu ya mchezo wa Taifa Stars.
    Vigumu kuelewa, hii Bodi ya Ligi imekuja kuboresha au ‘kuikongoloa’ Ligi Kuu? Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BODI YA LIGI IMEKUJA KUIBORESHA, AU ‘KUIKONGOLOA’ LIGI KUU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top