• HABARI MPYA

    Sunday, September 21, 2014

    MALINZI ASIKUBALI KUAMBIWA ANAENDESHA MAMBO KISWAHILI

    KWA miaka mingi, soka ya Tanzania imekuwa ya kutufurahisha wenyewe hapa hapa, haiwezi kuvuka mipaka kimataifa.
    Tanzania ilipata uanachama wa FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) miaka ya 1960, lakini hadi sasa imecheza fainali moja tu za mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Hilo ndilo kubwa la kujivunia na wachezaji wa wakati huo wanaonekana ‘malaika haswa’- wakati nchi ndogo ndogo kama Togo na Angola tayari zina historia ya kucheza Kombe la Dunia.
    Kila siku naitafuta maana ya Uswahili, neno ambalo limekuwa likitumika mno miongoni mwetu katika kubeza baadhi ya mambo ambayo si ya kitaaluma ambayo tunayaendekeza.

    Tunafanya mambo Kiswahili, tatizo letu ni uswahili- yaani maana yake kwa haraka haraka unaweza kusema ni kuendesha mambo bila kuzingatia weledi.
    Nini weledi maana yake? Weledi ni elimu ya uelewa juu ya suala husika, kwa mfano mtu aliyesomea kilimo, lazima atakuwa na weledi juu ya taaluma hiyo, huyo ukimpeleka kwenye teknolojia utaharibu.
    Vivyo hivyo katika michezo nchini, enzi za mwalimu Julius Nyerere (marehemu) taifa lilizalisha wataalamu wa michezo na lilikuwa lina wataalamu wa michezo na ndiyo maana wakati huo japokuwa hatukufikia mafanikio yenye kuonekana, lakini tulikuwa tunajitutumua licha ya kuachwa nyuma na teknolojia.
    Wataalamu hao wa michezo walisambazwa kuanzia shule za Msingi na somo elimu ya michezo kinadharia na vitendo lilianzia ngazi hiyo.
    Leo hii imekuwa tofauti mno, klabu zetu zimeshikwa na watu wenye fedha tu, lakini wengi hawana uelewa wa michezo na hawaujui mchezo kwa ujumla- ama wameingia kishabiki tu, kutafuta umaarufu au maslahi mengine.
    Lakini FIFA imerahisisha mambo, kwa kujua soka inahitaji fedha kuendeshwa, imetoa mwongozo wa kuwa na watendaji wa kuajiriwa wenye taaluma, weledi na uzoefu wa kutosha katika masuala ya michezo.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliipokea hiyo kama amri ya FIFA na kuiingiza katika klabu zetu kwa shinikizo, wakaipokea- lakini inasikitisha bado dhana yake haijaeleweka ipasavyo.
    Klabu zinajaribu kuwa na watendaji wa kuajiri ili kuiridhisha TFF na FIFA, lakini hazifikirii kuwa na watendaji wa aiana hiyo kwa ajili ya kuleta ufanisi ndani ya klabu.
    Na ndiyo maana sasa, klabu kongwe nchini, Simba SC na Yanga SC zinashindwa kujitoa kwenye makwapa ya matajiri, kwa sababu hazijimudu wakati zina rasilimali tosha.
    Leo Yanga SC waambie lolote, lakini si Manji aondoke- kwa sababu hawaamini kama klabu inaweza kusimama bila yeye.
    Ni dhana potofu, Simba SC wana udhamini wa TBL kama Yanga SC, hawana tajiri wa aina ya Manji, lakini mambo yanakwenda vizuri tu, ingawa si kwa kiwango stahili. Sioni tofauti ya Yanga SC na Simba SC japokuwa klabu moja eti ina tajiri mkubwa. 
    Simba SC wale, ni klabu tajiri sana- kuwa na majengo mawili pale Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi ni rasilimali kubwa, lakini tazama uwekezaji uliofanywa pale wa migahawa na maduka ya nguo hauendani kabisa.
    Yanga SC nao wana jingo Kariakoo na pale Jangwani- wanayatumiaje?
    Ni uswahili mtupu tunaouita uswahili ambao bahati mbaya sasa unataka kwenda mbali zaidi 
    TFF wiki hii imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea tuhuma za hujuma kwa timu ya taifa, Taifa Stars katika mechi za kufuzu mashindano ya AFCON.
    TFF imesema pamoja na kutokuwa na uthibitisho wa tuhuma hizi nzito haiwezi kuzikalia kimya na itateua jopo la kuchunguza tuhuma hizi, ambalo litawahoji wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za TFF, watalazimika kutoa ushirikiano. 
    Na TFF imesema atakayeshindwa kutoa ushirikiano atachukuliwa hatua za kimaadili.
    Tanzania ilianza na Zimbabwe ikafuzu kwa ushindi wa jumla wa 3-2 ikishinda nyumbani 1-0 na kwenda kutoa sare ya 2-2 Harare.
    Katika mchezo wa mwisho wa kufuzu, Tanzania ikatolewa na Msumbiji, ikianza kulazimishwa sare ya 2-2 nyumbani na kwenda kufungwa 2-1 Maputo.
    Makosa yaliyofanywa na wachezaji wetu katika mchezo huo hadi kuwapa mabao Msumbiji ni makosa yale yale ambayo wamekuwa wakifanya siku zote hadi kwenye klabu zao.
    Msumbiji ni timu ambayo imekuwa ikitunyanyasa kwa muda sasa, tangu Alhaj Muhiddin Ahmed Ndolanga ‘Tyson’ anaitwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), lango la Taifa Stars linalindwa na akina Mwameja Mohamed, Steven Nemes na Joseph Katuba (sasa marehemu).
    Tangu tuna wachezaji ambao tunaamini ni bora zaidi akina Athumani China, Saidi Mwamba ‘Kizota’ (marehemu), Hussein Marsha na Nteze John Lungu.
    Msumbiji ilitufunga nyumbani, wakati Marcio Maximo amefanikiwa kuwaunganisha mashabiki wa Tanzania na kuwa kitu kimoja na kuisapoti timu yao kwa nguzu zote.
    Leo tunatolewa na Msumbiji, tunaanza kuleta dhana za kuhujumiwa- sitaki kubeza harakati za TFF chini ya rais wake, Jamal Malinzi, lakini naweza tu kusema kwangu haiingii akilini kama tumetolewa na Msumbiji kwa sababu ya hujuma.
    Nchi hii ina mambo mengi, niseme yote yanawezekana, lakini kwa kuzingatia matokeo halisi ya uwanjani, inaniwia vigumu kukubali eti tumefungwa na Msumbiji kwa hujuma.
    Kile ndio kilele cha uwezo wa wachezaji wetu, kuwania fainali zilizopita za AFCON tulitolewa na Msumbiji pia kwa matuta baada ya sare ya jumla ya nyumbani na uigenini, Mbwana Samatta akikosa penalti.
    Je, wakati huo Leodegar Tenga akiwa Rais wa TFF, tujiulize nani alimtumia Samatta aihujumu Stars kwa kukosa penalti? Kevin Yondan ni beki mzuri, lakini amekuwa akitoa ‘maboko’ tangu Simba hadi wakaanza kusema anatumiwa na Yanga SC. Amehamia Yanga SC nako anatoa maboko kama kawaida na katika watu ambao klabu hiyo inaamini walichangia kuwakosesha ubingwa msimu uliopita, beki huyo ni miongoni mwao.
    Na taarifa zaidi zinasema, kocha aliyeondoka Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm alipendekeza beki huyo asisajiliwe tena kwa kuwa amekuwa akirudia makosa yale yale siku zote.
    Huyo huyo Yondan ndiye makosa yake yaliigharimu Stars mbele ya Msumbiji, sasa tunachokitafiuta hapa ni nini?
    Naamini Jamal Malinzi anaweza kufanikiwa kuiletea maendeleo soka ya Tanzania, lakini vyema akatazama na njia anazotaka kutumia- asikubali kuambiwa anaendesha mambo Kiswahili. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI ASIKUBALI KUAMBIWA ANAENDESHA MAMBO KISWAHILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top