• HABARI MPYA

    Friday, September 26, 2014

    CHARLES BONIFACE MKWASA ‘MASTER’ AULA TFF

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA kocha wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa ameteuliwa kuwa Ofisa Mtaalamu wa Elimu ya Mafunzo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameithibitishia BIN ZUBEIRY kwamba Mkwasa amepewa nafasi hiyo baada ya kurejea kutoka Uarabuni, alipokwenda kufundisha klabu.
    Kwa upande wake, Mkwasa, maarufu kama Master kwa jina la utani tangu enzi zake anacheza nafasi ya kiungo Yanga SC na Taifa Stars, amesema kwamba amekwishaanza kazi yake hiyo mpya TFF na anatarajia kuifanya kwa ufanisi kwa sababu ana utaalamu nayo.
    Wenye bahazi zao hawakai juu ya mawe; Charles Boniface Mkwasa amepata kazi TFF

    Kuhusu Mkataba wake na Yanga SC, Mkwasa alisema kwamba wakati anakwenda Uarabuni alipewa likizo ya mwaka mmoja, lakini kwa sababu amerudi kabla ya muda huo ameona bora kukubali kazi hiyo ya TFF kuliko kukaa bure.
    “Kama Yanga SC watanihitaji kurudi kazini kabla ya muda huo, ni suala la kuzungumzika tu, kwa sababu TFF ipo kwa ajili ya maendeleo ya soka hapa nchini na Yanga ni klabu ya Tanzania,”amesema mume huyo wa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Dodoma, Betty Mkwasa, mtangazaji maarufu wa zamani wa Redio na Televisheni.
    Mkwasa alijiunga na Yanga SC Desemba mwaka jana akitokea Ruvu Shooting ya Pwani, lakini baada ya msimu Mei mwaka huu akaondoka pamoja na aliyekuwa kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mholanzi Hans va der Pluijm kwenda Uarabuni.
    Hata hivyo, baada ya muda mfupi wa kufanya kazi huko, Pluijm aliyemchukua Mkwasa kwenda naye huko- akatofautiana na uongozi wa timu na kusitishiwa mikataba.
    Wakati Pluijm alirejea Ghana anakoishi, Mkwasa alirudi nyumbani Tanzania na sasa anaibukia TFF..
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHARLES BONIFACE MKWASA ‘MASTER’ AULA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top