• HABARI MPYA

    Wednesday, August 20, 2014

    MAMBO YAIVA ZIARA YA REAL MADRID NCHINI… FIGO, OWEN NA KAREMEBU WATUA KESHO DAR

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MWANASOKA bora wa zamani wa dunia, Mreno Luis Filipe Madeira Caeiro Figo anatarajiwa kutua kesho na msafara wa kwanza ya magwiji wa Real Madrid tayari kwa mchezo dhidi ya magwiji wa Tanzania Agosti 23 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
    Figo ataongozana na nyota wengine wawili waliowika Real Madrid muongo uliopita, mshambuliaji Michael Owen aliyeshinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi Kombe la Dunia mwaka 1998 Ufaransa na mwanasoka bora wa Oceania mara mbili 1995 na 1998 Christian Karembeu.
    Figo aliyestaafu Mei 31 mwaka 2009, alipiga tuzo mbili mfululizo mwaka 2000, Mwanasoka Bora Ulaya na Dunia na anakuja Tanzania kuwakumbushia watu enzi zake anatamba Real Madrid.
    Figo anatua kesho Dar es Salaam

    Mapokezi makubwa yameandaliwa kwa ajili ya magwiji hao Real Madrid ambao sasa wanakuja kwa awali na hadi Agosti 22 kikosi kizima kitakuwa kimekamilika Dar es Salaam.
    Mkurugenzi wa makampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), Farough Baghozah ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba magwiji hao watapokewa kwa maandamano Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na kupelekwa hoteli ya Ladger Plaza, Bahari Beach.
    Kikosi cha magwiji wa Tanzania, kitakachomenyana na Real Madrid kinaendelea mazoezi Uwanja wa Karume kwa wiki sasa kwa ajili ya mchezo huo wa kihistoria.
    Makipa maarufu waliowahi kuwika nchini, Mwameja Mohamed na Manyika Peter wamejumuishwa katika kikosi cha Tanzania All Stars kitakachomenyana na magwiji hao wa Real Madrid. 
    Chini ya makocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ na Wasaidizi Freddy Felix Minziro na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, Daktari Mwanandi Mkwankemwa na viongozi Mtemi Ramadhani, Hassan Mnyenye, Omar Gumbo na Hamisi Kisiwa kikosi hicho kitaingia kambini Dar es Salaam kujiandaa kwa mchezo huo wa Agosti 23, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Wengine walioItwa ni mabeki Nsajigwa Shadrack, Mecky Mexime, Boniface Pawasa, John Mwansasu, 
    Abubakar Kombo, George Masatu, Habib Kondo, 
    Viungo Suleiman Matola, Shaaban Ramadhani, Salvatory Edward, Sabri Ramadhani ‘China’, Yussuf Macho, Abdul Mashine, Abdul Maneno, Mao Mkami, Steven Nyenge, Madaraka Suleiman, Akida Makunda na Mtwa Kihwelo.
    Washambuliaji ni Monja Liseki, Iddi Moshi, Dua Said, Emmanuel Gabriel, Said Maulid, Thomas Kipese, Nasor Mwinyi ‘Bwanga’, Edibilly Lunyamila, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Clement Kahbuka, 
    Madaraka Suleiman na Akida Makunda. 
    Wachezaji waliotamba kuanzia La Liga, wakacheza ligi nyingine za Ulaya, Kombe la Ulaya, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia waliowahi kuchezea Real Madrid watakuja nchini.
    Katika ziara hiyo, pamoja na kucheza mchezo wa kirafiki na kikosi maalum cha wachezaji nyota wa Tanzania Agosti 23, pia watafanya utalii katika vivutio mbalimbali, ikiwemo kupanda mlima Kilimanjaro.
    Miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kuja na Real nchini ni pamoja na Wanasoka Bora wa zamani wa Dunia, Mfaransa Zinadine Zidane, Mreno Luis Figo na Mbrazil, Ronaldo Lima.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAMBO YAIVA ZIARA YA REAL MADRID NCHINI… FIGO, OWEN NA KAREMEBU WATUA KESHO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top