• HABARI MPYA

    Wednesday, August 20, 2014

    HIZI NI SALAMU ZENU KUTOKA APR, MWAKA JUZI ILIFUKUZA MAFAZA WOTE, IKAOKOTA YOSSO

    MWAKA 2012 APR ilitolewa na Yanga SC katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kufungwa mabao 2-0.
    Yanga SC ilikutana na Azam FC katika Fainali na kutwaa Kombe, huku APR wakishindwa kupata hata nafasi ya tatu baada ya kufungwa 2-1 na AS Vita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Awali, katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huo, APR ilitolewa mapema pia.  
    APR au Armee Patriotique Rwandaise, yaani Jeshi la Rwanda baada ya matokeo hayo, ikafanya kikao na wachezaji wake mjini Kigali.

    Hii ni timu ya Jeshi, ambayo inaongoza kulipa vizuri hapa Rwanda na kuhudumia wachezaji- lakini kitendo cha kushindwa kufika hata nafasi ya tatu Kombe la Kagame, kiliukera uongozi wa jeshi chini ya Jenerali Alex Kagame, Rais wa timu.
    Wakawaambia wachezaji, wanalipwa vizuri, kwenye Ligi ya Mabingwa hawafiki mbali, hata mashindano ya CECAFA nako wanashindwa?
    Wakawaambia kama ni hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwa nao- bora watengeneze timu mpya ya vijana wadogo, taratibu itaimarika.
    APR iliacha wachezaji ambao Tanzania walikuwa wanazitoa udenda timu zetu, Simba, Yanga na Azam akina Meddie Kegere, Mbuyu Twite, Kabange Twite, Leonel Saint- Preux na mastaa wengine ambao wakati huo walikuwa wanatamba hadi timu ya taifa, Amavubi. 
    Baada ya hapo, ikaunda timu yake kwa wachezaji vijana ambao walikuwepo kwenye kikosi cha timu ya vijana ya nchi hiyo chini ya umri wa miaka 17 kilichocheza Fanali za Kombe la Dunia mwaka 2011 nchini Mexico.
    Timu hiyo ilicheza michuano hiyo ya dunia ya vijana kwa kwa mara ya kwanza mwaka 2011, baada ya kushika nafasi ya pili katika michuano ya Afrika mwaka 2011, ambayo wao walikuwa wenyeji. 
    Pamoja na kutolewa katika hatua ya makundi, baada ya kufungwa na England na Uruguay, kabla ya kutoa sare na Canada, lakini vijana walipata uzofu mkubwa.
    Uongozi wa Jeshi la Rwanda, ukawabeba vijana hao kwa wingi katika timu yao na msimu wa Ligi Kuu ulipoanza, hawakufanya vizuri.
    Walimaliza Ligi Kuu katika nafasi ya sita na wakachekwa sana, kiasi cha mashabiki wao wenyewe kuanza kuisusa timu, wakawa hawaendi uwanjani inapocheza.
    Uongozi wa timu ukaendelea kuwavumilia vijana, ukiamini ipo siku watarejesha heshima ya APR. Haikuchukua muda, msimu uliofuata APR ikawa tishio tena, baada ya yosso wake kukomaa.
    Ilizipiku timu zote za Ligi Kuu na kutwaa ubingwa wa Rwanda- hivyo ikapata tiketi ya kucheza Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tena mwaka huu nyumbani.
    Baada ya kuongoza kundi lao, B Kombe la Kagame, APR wakakutana na Rayon Sport ambayo inaundwa na wachezaji wazoefu wakiwemo wa kigeni katika Robo Fainali jana.
    APR imekwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa penalti 4-3 baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 na sasa itakutana na timu nyingine ya Rwanda, yenye wachezaji wazoefu pia, Polisi.
    Mashabiki wa APR wameanza kufurahia tena timu yao na sasa wanaimba majina ya yosso ambao awali waliwadharau na kususa kwenda uwanjani.
    Haya ni matunda ya uvumilivu na misimamo ambayo walikuwa nayo viongozi wa APR. Sasa hata Amavubi, timu ya taifa ya Rwanda inategemea wachezaji wengi wa APR.
    Najiuliza, kama wale watoto wa U17 ya Rwanda baada ya kurejea kutoka Kombe la Dunia kule Mexico, kila timu ingewadharau- leo wangekuwa wapi?
    Si ndiyo yangekuwa yale yale ya Watanzania, kila siku wanauliza, “Wale watoto waliokwenda Brazil na Afrika Kusini Copa Coca Cola wako wapi?”.
    Bajeti ya uendeshaji APR imepungua kwa kiasi kikubwa kwa kutumia wachezaji wa nyumbani tena vijana wadogo.
    Sasa tayari wazee ‘mteremko’ Simba na Yanga zetu wamekwishaanza kuwamezea mate na hawa hawa yosso wa APR- Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe yupo huku Rwanda anasotea saini ya beki Emery Bayisenga aliyekuwa Nahodha wa timu kule Mexico.
    Kila la heri kwake ZHP, lakini habari zilizopo ni kwamba, kwa sasa APR ‘Hawauzi mbuzi wao’- baada ya kuyatoa yale magumegume yaliyokuwa yanakula mishahara ya bure na sasa jicho lao lipo kwa yosso hawa wa Mexico. Hizi ndizo salamu kutoka APR, ambazo leo nimependa kuwaletea wapendwa wasomaji wangu. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIZI NI SALAMU ZENU KUTOKA APR, MWAKA JUZI ILIFUKUZA MAFAZA WOTE, IKAOKOTA YOSSO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top