• HABARI MPYA

    Tuesday, August 19, 2014

    HANS POPPE AFANYA YAKE KIGALI, BEKI LA BURUNDI LAPANDA NDEGE KESHO KWENDA DAR KUJIUNGA NA SIMBA SC

    Na Mahmoud Zubeiry, KIGALI
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe anampandisha ndege kesho beki wa Telecom ya Djibouti, Butoyi Hussein kwenda Dar es Salaam, baadaye kambini Zanzibar kutazamwa na kocha Patrick Phiri.
    Poppe amevutiwa mno na uchezaji wa beki huyo wa kati Mrundi na ameamua kutoa fedha za kumgharimia safari ya Tanzania ili akatazamwe na kocha Phiri- kama akifaa atapewa Mkataba.
    Uzuri zaidi, beki huyo amemaliza Mkataba wake na Telecom, hivyo akifanikiwa Simba SC klabu haitahitaji fedha za kumhamisha zaidi ya kupatana na mchezaji mwenyewe pekee.
    Hakuna kulala; Hans Poppe katikati akiwa na beki wa Telecom, Butoyi Hussein kulia na kushoto ni kipa wa timu hiyo, Jeef Inzokira aliyemsindikiza mwenzake kuzungumza na bosi

    Poppe aliibuka mjini Kigali, Rwanda mwishoni mwa wiki ambako michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inaendelea na Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amekuwa akihudhuria Uwanja wa Nyamirambo na ndiko alipomuona Butoyi.
    Poppe alitua Kigali, baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza kwa siku 10 muda wa kumalizika usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL)  kutokana na kuchelewa kwa link ya mfumo mpya wa usajili (system) kutoka Shirikisho la Soka Miguu Afrika (CAF).
    Kwa mujibu wa CAF, link hiyo itakuwa tayari kwa matumizi ndani ya siku tatu zijazo kutokana sasa. Hivyo, mameneja wa usajili wa timu hizo kwa sasa wanatakiwa kukamilisha nyaraka zote zinazotakiwa ili link hiyo itakapokuwa tayari waweze kuingiza usajili wao mara moja.
    Kuanzia msimu wa 2014/2015 mfumo unaotumika kwa usajili kwa klabu hizo ni wa elektroniki badala ya ule wa zamani wa kutumia fomu za kawaida. Mfumo huo wa kisasa ambao pia unatumiwa na CAF unaondoa upungufu uliokuwepo katika mfumo wa zamani.
    Kutokana na mabadiliko hayo, usajili sasa utamalizika Agosti 27 mwaka huu badala ya leo (Agosti 17 mwaka huu). Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Agosti 28 mwaka huu hadi Septemba 3 mwaka huu.
    Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakutana kati ya Septemba 6 na 8 mwaka huu kwa ajili ya kupitia pingamizi na kuthibitisha usajili.
    Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoshirikisha timu 14 itaanza Septemba 20 mwaka huu wakati ratiba inatarajia kutoka mwezi mmoja kabla ya kuanza ligi hiyo. Ligi Daraja la Kwanza inatarajia kuanza wiki ya kwanza ya Oktoba.
    Mwisho wa kuombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa wachezaji wanatoka nje ya Tanzania ni Septemba 6 mwaka huu.
    Hata hivyo, Simba SC tayari ina wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, ambao ni mabeki Mganda, Joseph Owino, Mkenya, Donald Mosoti, Warundi kiungo Pierre Kwizera na Amisi Tambwe pamoja na mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera.  
    Pamoja na hayo, kumekuwa na tetesi kwamba idadi ya wachezaji wa kigeni itaongezwa kutoka watano hadi saba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE AFANYA YAKE KIGALI, BEKI LA BURUNDI LAPANDA NDEGE KESHO KWENDA DAR KUJIUNGA NA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top