• HABARI MPYA

    Monday, August 18, 2014

    FIFA KUIJENGEA OFISI BABU KUBWA TFF YA MALINZI

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limeahidi kuboresha makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yaliyoko kwenye Uwanja wa
    Kumbukumbu ya Karume, Ilala ili yawe katika kiwango cha kisasa ikiwa ni pamoja na kuwa na vitendea kazi na miundombinu ikiwa ni pamoja na upanuzi wa ofisi.
    Hatua hiyo itaiwezesha TFF kuwa na mazingira bora ya kufanya shughuli zake kwa ufanisi. Vilevile kupitia programu zake mbalimbali ikiwemo ile ya Goal, FIFA imeahidi kushirikiana na TFF katika kuendeleza mradi wa kiuchumi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi 

    Mwanzoni mwa mwaka huu, TFF ilihamishia makao yake makuu katikati ya jiji ili kupisha maendeleo ya kuiwezesha Karume kuwa kituo cha kisasa kwa
    michezo na vitega uchumi.
    Akiongea mwishoni mwa ziara ya kikazi nchini, Meneja Miradi wa FIFA anayeshughulikia Programu za Afrika, Zelkifli Ngoufonja amesema FIFA inaunga mkono wazo la kuboresha makao makuu ya Karume na itasaidia kwa awamu uboreshaji huo.
    Katika kuhakikisha usimamizi na utekelezaji
    barabara wa mradi huo, ujumbe huo wa FIFA ulikubaliana na Kamati ya Utendaji ya TFF kuboresha ofisi za Karume ili jengo la utawala lianze
    kutumika huku mradi ukitekelezwa kwa awamu.
    Pamoja na kuongelea mradi huo muhimu kimichezo na kibiashara, ujumbe huo uliokuwa nchini kwa juma moja kufuatia mwaliko wa TFF ulikuwa na nafasi ya kujadiliana na TFF kuhusu maboresho katika masuala mbalimbali yakiwemo ya
    Utawala, Fedha, Masoko, Ufundi, Mashindano na timu za taifa.
    Akiongea kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Rais wa TFF Jamal Malinzi aliushukuru ujumbe huo wa FIFA kwa msaada mkubwa katika historia ya
    mahusiano kati ya FIFA na TFF.
    Ujio huo unafuatia maombi ya TFF kuwa sehemu ya mradi wa Performance wa FIFA. Mradi wa Performance unaoshirikisha nchi mashirikisho 163 kati ya wanachama 209 wa FIFA, unalenga kuongeza ufanisi katika uendeshaji na uongozi wa nchi wanachama wa FIFA.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA KUIJENGEA OFISI BABU KUBWA TFF YA MALINZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top