• HABARI MPYA

    Wednesday, August 27, 2014

    COUTINHO APIGA BONGE LA BAO YANGA SC IKIICHAPA KMKM 2-0 AMAAN

    Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
    YANGA SC imemaliza ziara yake ya kisiwani Unguja kwa ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM, Uwanja wa Amaan, Zanzibar usiku huu.
    Mabao ya Yanga SC hii leo yamefungwa na Mbrazil, Andrey Coutinho na mzalendo Hussein Javu, moja kila kipindi.
    Lakini lilikuwa ni bao la Coutinho lililosisimua zaidi usiku huu, akifumua shuti la umbali wa mita 25 baada ya kupata pasi maridadi ya Mrisho Ngassa dakika ya 44.
    Bao la pili pia lilipatikana dakika ya 89 na ushei baada ya Javu kufumua shuti la mbali pia, ambalo kipa wa KMKM hakuliona.
    Mkali kweli; Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza mwenzao, Andrey Coutinho baada ya kufunga bao la kwanza
    Coutinho akimlamba chenga beki wa KMKM usiku huu Uwanja wa Amaan

    Kama ilivyokuwa katika mchezo dhidi ya Shangani, na leo pia kocha Mbrazil, Marcio Maximo alibadili kikosi kizima kipindi cha pili, akimuacha mchezaji mmoja tu, Kevin Yondan. 
    Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Amos Abel ambao waliingia kipindi cha pili, baadaye walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Said Bahanuzi, Edward Charles na Javu.
    Tegete alikosa mabao mawili ya wazi baada ya pasi nzuri za Simon Msuva akiwa ndani ya eneo la sita na bila shaka hilo ndilo lililomfanya Maximo amrejeshe benchi.
    Kwa mara nyingine, mshambuliaji Mbrazil, Geilson Santana ‘Jaja’ ameshindwa kufurukuta huku Coutinho akiendelea kudhihirisha ubora wake.
    Huo unakuwa mchezo wa tatu kwa ujumla Yanga SC kucheza visiwani hapa na inashinda mechi zote, 1-0 dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani, Pemba na 2-0 dhidi ya Shangani Uwanja wa Amaan pia.
    Yanga SC inatarajiwa kuondoka kesho mjini hapa kurejea Dar es Salaam kwa maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii, dhidi ya Azam FC Septemba 13, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’/Juma Kaseja dk46, Salum Telela/Said Juma dk46, Oscar Joshua/Amos Abel dk46/Edward Charles dk70, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Rajab Zahir dk46, Mbuyu Twite/Omega Seme dk46, Mrisho Ngassa/Simon Msuva dk46, Hassan Dilunga/Nizar Khalfan dk46, Geilson Santana ‘Jaja’/Jerry Tegete dk46/Said Bahanuzi dk70, Haruna Niyonzima/Hamisi Thabiti dk46 na Andrey Coutinho/Hamisi Kiiza/Hussein Javu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: COUTINHO APIGA BONGE LA BAO YANGA SC IKIICHAPA KMKM 2-0 AMAAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top